Categories
2 Wakorintho

2 Wakorintho 6

1 Kama watendakazi pamoja na Mungu, tunawasihi msipokee neema ya Mungu bure.

2 Kwa maana asema:

“Wakati wangu uliokubalika nilikusikia,

siku ya wokovu nilikusaidia.”

Tazama, wakati uliokubalika ndio huu, siku ya wokovu ndiyo sasa.

Taabu Za Paulo

3 Hatuweki kitu cha kukwaza katika njia ya mtu yeyote, ili huduma yetu isionekane kuwa na lawama.

4 Bali kama watumishi wa Mungu tuonyeshe kwa kila njia: katika saburi nyingi; katika dhiki, katika misiba, na katika shida;

5 katika kupigwa, katika kufungwa gerezani na katika ghasia; katika kazi ngumu, katika kukesha na katika kufunga;

6 katika utakatifu, katika ufahamu, katika uvumilivu, na katika utu wema; katika Roho Mtakatifu na upendo wa kweli;

7 katika maneno ya kweli na katika nguvu za Mungu, kwa silaha za haki za mkono wa kuume na za mkono wa kushoto;

8 katika utukufu na katika kudharauliwa; katika sifa mbaya na katika sifa nzuri; tukiwa kama wadanganyaji, lakini tukiwa wakweli;

9 tukiwa maarufu, lakini tukihesabiwa kama tusiojulikana; tukiwa kama wanaokufa, lakini tunaishi; tukipigwa, lakini hatuuawi;

10 tukiwa kama wenye huzuni, lakini siku zote tukifurahi; tukionekana maskini, lakini tukitajirisha wengi; tukiwa kama wasio na kitu, lakini tuna vitu vyote.

11 Tumesema nanyi wazi, enyi Wakorintho na kuwafungulieni mioyo yetu wazi kabisa.

12 Sisi hatujizuii kuwapenda, bali ninyi mmeuzuia upendo wenu kwetu.

13 Sasa nasema, kama na watoto wangu: Ninyi pia ifungueni mioyo yenu kabisa.

Msifungiwe Nira Pamoja Na Wasioamini

14 Msifungiwe nira pamoja na watu wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa, kwa maana pana uhusiano gani kati ya haki na uovu? Au kuna ushirika gani kati ya nuru na giza?

15 Kuna mapatano gani kati ya Kristo na Beliari?Yeye aaminiye ana sehemu gani na yeye asiyeamini?

16 Kuna mapatano gani kati ya Hekalu la Mungu na sanamu? Kwa kuwa sisi tu Hekalu la Mungu aliye hai. Kama Mungu alivyosema: “Nitakaa pamoja nao na kutembea katikati yao, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.”

17 “Kwa hiyo tokeni miongoni mwao,

mkatengwe nao,

asema Bwana.

Msiguse kitu chochote kilicho najisi,

nami nitawakaribisha.”

18 “Mimi nitakuwa Baba kwenu,

nanyi mtakuwa wanangu na binti zangu,

asema Bwana Mwenyezi.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/2CO/6-5a25b68d5d369fa2494ad0f73ea721b9.mp3?version_id=1627—

Categories
2 Wakorintho

2 Wakorintho 7

1 Wapenzi, kwa kuwa tunazo ahadi hizi, basi na tujitakase nafsi zetu kutokana na kila kitu kitiacho mwili na roho unajisi, tukitimiza utakatifu kwa kumcha Mungu.

Furaha Ya Paulo

2 Tupatieni nafasi mioyoni mwenu. Hatujamkosea mtu yeyote, hatujampotosha mtu yeyote, wala hatujamdhulumu mtu yeyote.

3 Sisemi haya ili kuwahukumu, kwa kuwa nilisema mwanzo, kwamba ninyi mko mioyoni mwetu hata kwa kufa pamoja au kuishi pamoja.

4 Mara nyingi najivuna kwa ajili yenu; naona fahari juu yenu. Nimejawa na faraja. Nina furaha kupita kiasi katika mateso yetu yote.

5 Kwa maana hata tulipoingia Makedonia, miili yetu haikuwa na raha. Tulisumbuliwa kila upande, kwa nje kulikuwa na mapigano na mioyoni mwetu tulikuwa na hofu.

6 Bali Mungu, yeye awafarijie wenye huzuni, alitufariji kwa kufika kwake Tito.

7 Lakini si kule kuja kwa Tito tu, bali pia kwa faraja mliyompa. Alitueleza jinsi mlivyonionea shauku, huzuni yenu kubwa na juhudi yenu kwa ajili yangu, ili kwamba furaha yangu ipate kuwa kubwa kuliko wakati wowote.

8 Hata kama niliwahuzunisha kwa barua yangu, sijutii. Ingawa nilijuta kwa muda mfupi, kwa kuwa najua kwamba barua yangu iliwaumiza, lakini ni kwa kitambo tu,

9 lakini sasa nina furaha, si kwa sababu mlihuzunika, bali kwa kuwa huzuni hiyo iliwafanya mtubu. Kwa maana mlihuzunishwa kama Mungu alivyokusudia watu wahuzunike na hivyo sisi hatukuwadhuru kwa njia yoyote.

10 Kwa maana huzuni ya kimungu huleta toba iletayo wokovu na wala haina majuto. Lakini huzuni ya kidunia husababisha mauti.

11 Tazameni jinsi huzuni hii ya kimungu ilivyoleta faida ndani yenu: bidii mliyo nayo, juhudi mliyofanya kujitetea, uchungu wenu, hofu yenu, upendo wenu, shauku yenu na jinsi mlivyokuwa tayari kutoa adhabu inayostahili. Kwa kila njia mmejithibitisha kuwa safi katika jambo hilo.

12 Hivyo ingawa niliwaandikia, haikuwa kwa sababu ya huyo aliyekosa au huyo aliyekosewa. Lakini nilitaka ninyi wenyewe mwone, mbele za Mungu, jinsi mlivyojitoa kwa ajili yetu.

13 Kwa ajili ya haya tumefarijika.

Zaidi ya kule sisi kutiwa moyo, tulifurahi sana kumwona Tito alivyo na furaha, kwa sababu roho yake imeburudishwa na ninyi nyote.

14 Nilikuwa nimewasifu ninyi kwake, nanyi hamkuniaibisha. Lakini kila kitu tulichowaambia ninyi, kilikuwa kweli, hivyo kule kujisifu kwetu kwa Tito kuwahusu ninyi kumethibitishwa kuwa kweli pia.

15 Upendo wake kwenu unaongezeka sana anapokumbuka jinsi mlivyokuwa watiifu, na kumpokea kwa hofu na kutetemeka.

16 Nafurahi kwamba ninaweza kuwatumaini ninyi kabisa.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/2CO/7-ee01df6f73bfcd00096b70d6c901b279.mp3?version_id=1627—

Categories
2 Wakorintho

2 Wakorintho 8

Kutoa Kwa Ukarimu

1 Basi sasa ndugu, nataka ninyi mjue kuhusu ile neema ambayo Mungu amewapa makanisa ya Makedonia.

2 Pamoja na majaribu makali na taabu walizopata, furaha waliyokuwa nayo ilikuwa kubwa, ingawa walikuwa maskini kupindukia, kwa upande wao walifurika kwa wingi wa ukarimu.

3 Kwa maana nashuhudia kwamba wao walitoa kwa kadiri wawezavyo, hata na zaidi ya uwezo wao, kwa hiari yao wenyewe,

4 wakitusihi kwa bidii wapewe fursa ya kushiriki katika huduma hii ya kuwasaidia watakatifu.

5 Wala hawakufanya tulivyotazamia, bali walijitoa wao wenyewe kwa Bwana kwanza na ndipo wakajitoa kwa ajili yetu, kufuatana na mapenzi ya Mungu.

6 Kwa hiyo tulimsihi Tito, kwa kuwa ndiye alianzisha jambo hili, akamilishe tendo hili la neema kwa upande wenu.

7 Lakini kama vile mlivyo mbele sana katika yote: Katika imani, katika usemi, katika maarifa, katika uaminifu wote na katika upendo wenu kwetu sisi, vivyo hivyo tunataka pia mzidi katika neema hii ya kutoa.

8 Siwaamrishi, lakini nataka kujaribu unyofu wa upendo wenu kwa kuulinganisha na bidii ya wengine.

9 Kwa maana mnajua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba ingawa alikuwa tajiri, kwa ajili yenu alikubali kuwa maskini, ili kwa umaskini wake ninyi mpate kuwa matajiri.

10 Ushauri wangu kuhusu lile lililo bora kwenu juu ya jambo hili ni huu: Mwaka uliopita ninyi mlikuwa wa kwanza si tu kutoa lakini pia mlikuwa na shauku ya kufanya hivyo.

11 Sasa ikamilisheni kazi hii kwa shauku kama mlivyoanza, jitoleeni kulingana na uwezo wenu.

12 Kwa kuwa kama nia ya kutoa ipo, kitolewacho kinakubalika kulingana na kile mtu alicho nacho, wala si kwa kile ambacho hana.

13 Nia yetu si kwamba wengine wasaidike wakati ninyi mnateseka, bali pawe na uwiano.

14 Kwa wakati huu, wingi wa vitu mlivyo navyo usaidie kutosheleza mahitaji yao, ili wakati wao watakapokuwa na wingi wa vitu, nao wapate kutosheleza mahitaji yenu.

15 Ndipo patakuwa na usawa, kama ilivyoandikwa: “Aliyekusanya zaidi hakuwa na ziada, wala aliyekusanya kidogo hakupungukiwa.”

Tito Atumwa Korintho

16 Ninamshukuru Mungu ambaye amemtia Tito moyo wa kuwajali ninyi kama mimi ninavyowajali.

17 Si kwamba Tito amekubali tu ombi letu, bali anakuja kwenu akiwa na shauku kuliko wakati mwingine, tena kwa hiari yake mwenyewe.

18 Nasi tunamtuma pamoja naye ndugu ambaye anasifiwa na makanisa yote kwa huduma yake ya kuhubiri Injili.

19 Zaidi ya hayo, alichaguliwa na makanisa ili asafiri pamoja nasi tulipokuwa tunapeleka matoleo ya ukarimu, kwa ajili ya utukufu wa Bwana mwenyewe, na ili kuonyesha hisani yetu kuwasaidia.

20 Tunataka kuepuka lawama yoyote kuhusu jinsi tunavyosimamia matoleo haya ya ukarimu.

21 Kwa kuwa tunakusudia kufanya kile kilicho haki si machoni mwa Bwana peke yake, bali pia machoni mwa watu wengine.

22 Pamoja nao, tunamtuma ndugu yetu ambaye mara kwa mara ametuthibitishia kwa njia nyingi kwamba ana shauku, naam, zaidi sana sasa kwa sababu analo tumaini kuu kwenu.

23 Kwa habari ya Tito, yeye ni mwenzangu na mtendakazi pamoja nami miongoni mwenu. Kwa habari za ndugu zetu, wao ni wawakilishi wa makanisa, na utukufu kwa Kristo.

24 Kwa hiyo waonyesheni wazi hawa ndugu uthibitisho wa upendo wenu na sababu inayotufanya tujivune kwa ajili yenu, mbele ya makanisa, ili yapate kuona.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/2CO/8-7dfa9218cbb988bf678b0483c6c19c43.mp3?version_id=1627—

Categories
2 Wakorintho

2 Wakorintho 9

Wasaidieni Wakristo Wenzenu

1 Hakuna haja yangu kuwaandikia kuhusu huduma hii itolewayo kwa ajili ya watakatifu.

2 Kwa kuwa ninajua mlivyo na shauku ya kusaidia, nami nimekuwa nikijivuna kwa ajili ya jambo hilo kwa watu wa Makedonia, nikiwaambia kuwa ninyi wa Akaya mmekuwa tayari kutoa tangu mwaka jana na shauku yenu imewachochea wengi wao katika kutoa.

3 Lakini sasa nawatuma hawa ndugu ili kujivuna kwetu kuhusu mchango wenu kusiwe maneno matupu, bali mpate kuwa tayari kama nilivyosema mngekuwa tayari.

4 Kwa maana kama nikija na Mmakedonia yeyote na kuwakuta hamjawa tayari, tutaona aibu kusema chochote juu yenu katika matoleo.

5 Kwa hivyo niliona ni muhimu niwahimize hawa ndugu watangulie kuja huko kwenu kabla yangu, wafanye mipango ya hayo matoleo ya ukarimu mliyokuwa mmeahidi, ili yawe tayari kama matoleo ya hiari wala si kama ya kutozwa kwa nguvu.

Kupanda Kwa Ukarimu

6 Kumbukeni kwamba: Yeyote apandaye kwa uchache pia atavuna kwa uchache, naye apandaye kwa ukarimu pia atavuna kwa ukarimu.

7 Kila mtu atoe kama anavyokusudia moyoni mwake, si kwa uchoyo au kwa kulazimishwa, kwa maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo mkunjufu.

8 Naye Mungu aweza kuwapa kila baraka kwa wingi, ili katika mambo yote kila wakati, mwe na kila kitu mnachohitaji, ili mweze kushiriki kwa wingi katika kila kazi njema.

9 Kama ilivyoandikwa:

“Ametawanya vipawa vyake kwa ukarimu

akawapa maskini;

haki yake hudumu milele.”

10 Yeye ampaye mpanzi mbegu kwa ajili ya kupanda na mkate kuwa chakula, atawapa na kuzizidisha mbegu zenu za kupanda na kuongeza mavuno ya haki yenu.

11 Mtatajirishwa kwa kila namna ili mpate kuwa wakarimu kila wakati, na kupitia kwetu, ukarimu wenu utamletea Mungu shukrani.

12 Huduma hii mnayofanya si tu kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya watakatifu, bali huzidi sana kwa shukrani nyingi apewazo Mungu.

13 Kwa sababu ya huduma ambayo mmejithibitisha wenyewe, watu watamtukuza Mungu kwa ajili ya utiifu ufuatanao na ukiri wenu wa Injili ya Kristo, na kwa ukarimu wenu wa kushiriki pamoja nao na pia wengine wote.

14 Nao katika maombi yao kwenu mioyo yao itawaonea shauku kwa sababu ya neema ipitayo kiasi mliyopewa na Mungu.

15 Ashukuriwe Mungu kwa karama yake isiyoelezeka.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/2CO/9-81d751a0e9effc3a1acf18fca42f3c82.mp3?version_id=1627—

Categories
2 Wakorintho

2 Wakorintho 10

Paulo Atetea Huduma Yake

1 Basi, mimi Paulo ninawasihi kwa unyenyekevu na upole wa Kristo, mimi niliye “mwoga” ninapokuwa pamoja nanyi ana kwa ana, lakini mwenye ujasiri nikiwa mbali nanyi!

2 Nawaomba nitakapokuja kwenu nisiwe na ujasiri dhidi ya watu fulani, kama ninavyotazamia kwa wale wanaodhani kwamba tunaishi kwa kufuata namna ya ulimwengu huu.

3 Ingawa tunaishi duniani, hatupigani vita kama ulimwengu ufanyavyo.

4 Silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome,

5 tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu, na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo,

6 tena tukiwa tayari kuadhibu kila tendo la kutotii, kutii kwenu kutakapokamilika.

7 Angalieni yale yaliyo machoni penu. Kama mtu yeyote anaamini kuwa yeye ni mali ya Kristo, basi kumbuka kuwa kama ulivyo wa Kristo, vivyo hivyo na sisi ndivyo tulivyo.

8 Basi hata kama nikijisifu zaidi kidogo kuhusu mamlaka tuliyo nayo, ambayo Bwana alitupa ili kuwajenga wala si kuwabomoa, mimi sitaionea haya.

9 Sitaki nionekane kama ninayejaribu kuwatisha kwa nyaraka zangu.

10 Kwa maana wanasema, “Nyaraka zake ni nzito na zenye nguvu, lakini ana kwa ana ni dhaifu na kuzungumza kwake ni kwa kudharauliwa.”

11 Watu kama hao wajue ya kuwa, yale tusemayo kwa barua tukiwa hatupo pamoja nanyi, ndivyo tulivyo na ndivyo tutakavyofanya tutakapokuwa pamoja nanyi.

12 Hatuthubutu kujiweka kwenye kundi moja au kujilinganisha na hao wanaojitukuza wenyewe kuwa wao ni wa maana sana. Wanapojipima na kujilinganisha wenyewe kwa wenyewe, wanaonyesha ya kuwa hawana busara.

13 Lakini sisi hatujajivuna kupita kiasi, bali majivuno yetu yatakuwa katika mipaka ile Mungu aliyotuwekea, mipaka ambayo inawafikia hata ninyi.

14 Kwa maana hatukuwa tunavuka mipaka katika kujisifu kwetu, kama vile ambavyo ingekuwa kama hatukuwa tumekuja kwenu. Kwa maana sisi ndio tuliokuwa wa kwanza kuja kwenu na Injili ya Kristo.

15 Wala hatuvuki mipaka kwa kujisifu kwetu kwa ajili ya kazi iliyofanywa na watu wengine. Tumaini letu ni kwamba imani yenu inavyozidi kukua, eneo letu la utendaji miongoni mwenu litapanuka zaidi,

16 ili tuweze kuhubiri Injili sehemu zilizo mbali na maeneo yenu. Kwa maana hatutaki kujisifu kwa ajili ya kazi ambayo imekwisha kufanyika tayari katika eneo la mtu mwingine.

17 Lakini, “Yeye ajisifuye na ajisifu katika Bwana.”

18 Kwa maana si yeye ajisifuye mwenyewe akubaliwaye, bali yeye ambaye Bwana humsifu.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/2CO/10-b86656ecaf36cde5a35f97e627184184.mp3?version_id=1627—

Categories
2 Wakorintho

2 Wakorintho 11

Paulo Na Mitume Wa Uongo

1 Laiti mngenivumilia kidogo katika upumbavu wangu! Naam, nivumilieni kidogo.

2 Ninawaonea wivu, wivu wa Kimungu, kwa kuwa mimi niliwaposea mume mmoja, ili niwalete kwa Kristo kama mabikira safi.

3 Lakini nina hofu kuwa, kama vile Eva alivyodanganywa kwa ujanja wa yule nyoka, mawazo yenu yasije yakapotoshwa, mkauacha unyofu na usafi wa upendo wenu kwa Kristo.

4 Kwa sababu kama mtu akija na kuwahubiria Yesu mwingine ambaye si yule tuliyemhubiri, au kama mkipokea roho mwingine ambaye si yule mliyempokea, au Injili tofauti na ile mliyoikubali, ninyi mnaitii kwa urahisi.

5 Lakini sidhani ya kuwa mimi ni dhalili sana kuliko hao “mitume wakuu.”

6 Inawezekana mimi nikawa si mnenaji hodari, lakini ni hodari katika elimu. Jambo hili tumelifanya liwe dhahiri kwenu kwa njia zote.

7 Je, nilitenda dhambi kwa kujishusha ili kuwainua ninyi kwa kuwahubiria Injili ya Mungu pasipo malipo?

8 Niliyanyangʼanya makanisa mengine kwa kupokea misaada kutoka kwao ili niweze kuwahudumia ninyi.

9 Nami nilipokuwa pamoja nanyi, nikipungukiwa na chochote, sikuwa mzigo kwa mtu yeyote, kwa maana ndugu waliotoka Makedonia walinipatia mahitaji yangu. Kwa hiyo nilijizuia kuwa mzigo kwenu kwa njia yoyote, nami nitaendelea kujizuia.

10 Kwa hakika kama vile kweli ya Kristo ilivyo ndani yangu, hakuna mtu yeyote katika Akaya nzima atakayenizuia kujivunia jambo hili.

11 Kwa nini? Je, ni kwa sababu siwapendi? Mungu anajua ya kuwa nawapenda!

12 Nami nitaendelea kufanya lile ninalofanya sasa ili nisiwape nafasi wale ambao wanatafuta nafasi ya kuhesabiwa kuwa sawa na sisi katika mambo wanayojisifia.

13 Watu kama hao ni mitume wa uongo, ni wafanyakazi wadanganyifu, wanaojigeuza waonekane kama mitume wa Kristo.

14 Wala hii si ajabu, kwa kuwa hata Shetani mwenyewe hujigeuza aonekane kama malaika wa nuru.

15 Kwa hiyo basi si ajabu, kama watumishi wa Shetani nao hujigeuza ili waonekane kama watumishi wa haki. Mwisho wao utakuwa sawa na matendo yao yanavyostahili.

Paulo Anajivunia Mateso Yake

16 Nasema tena, mtu yeyote asidhani kwamba mimi ni mjinga. Lakini hata kama mkinidhania hivyo, basi nipokeeni kama mjinga ili nipate kujisifu kidogo.

17 Ninayosema kuhusiana na huku kujisifu kwa kujiamini, sisemi kama vile ambavyo Bwana angesema, bali kama mjinga.

18 Kwa kuwa wengi wanajisifu kama vile ulimwengu ufanyavyo, mimi nami nitajisifu.

19 Ninyi mwachukuliana na wajinga kwa sababu mna hekima sana!

20 Kweli ni kwamba mnachukuliana na mtu akiwatia utumwani au akiwatumia kwa ajili ya kupata faida au akiwanyangʼanya au akijitukuza mwenyewe au akiwadanganya.

21 Kwa aibu inanipasa niseme kwamba sisi tulikuwa dhaifu sana kwa jambo hilo!

Lakini chochote ambacho mtu mwingine yeyote angethubutu kujisifia, nanena kama mjinga, nami nathubutu kujisifu juu ya hilo.

22 Je, wao ni Waebrania? Mimi pia ni Mwebrania. Je, wao ni Waisraeli? Mimi pia ni Mwisraeli. Je, wao ni wazao wa Abrahamu? Mimi pia ni mzao wa Abrahamu.

23 Je, wao ni watumishi wa Kristo? (Nanena kiwazimu.) Mimi ni zaidi yao. Nimefanya kazi kwa bidii kuwaliko wao, nimefungwa gerezani mara kwa mara, nimechapwa mijeledi sana, na nimekabiliwa na mauti mara nyingi.

24 Mara tano nimechapwa na Wayahudi viboko arobaini kasoro kimoja.

25 Mara tatu nilichapwa kwa fimbo, mara moja nilipigwa kwa mawe, mara tatu nimevunjikiwa na meli, nimekaa kilindini usiku kucha na mchana kutwa,

26 katika safari za mara kwa mara. Nimekabiliwa na hatari za kwenye mito, hatari za wanyangʼanyi, hatari kutoka kwa watu wangu mwenyewe, hatari kutoka kwa watu wa Mataifa; hatari mijini, hatari nyikani, hatari baharini; na hatari kutoka kwa ndugu wa uongo.

27 Nimekuwa katika kazi ngumu na taabu, katika kukesha mara nyingi; ninajua kukaa njaa na kuona kiu; nimefunga kula chakula mara nyingi; nimehisi baridi na kuwa uchi.

28 Zaidi ya hayo yote, nakabiliwa na mzigo wa wajibu wangu kwa makanisa yote.

29 Je, ni nani aliye mdhaifu, nami nisijisikie mdhaifu? Je, nani aliyekwazwa, nami nisiudhike?

30 Kama ni lazima nijisifu, basi nitajisifia yale mambo yanayoonyesha udhaifu wangu.

31 Mungu na Baba wa Bwana Yesu, yeye ambaye anahimidiwa milele, anajua ya kuwa mimi sisemi uongo.

32 Huko Dameski, mtawala aliyekuwa chini ya Mfalme Areta aliulinda mji wa Dameski ili kunikamata.

33 Lakini nilishushwa kwa kapu kubwa kupitia katika dirisha ukutani, nikatoroka kutoka mikononi mwake.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/2CO/11-5379cc770a4defa25352ac54c815a727.mp3?version_id=1627—

Categories
2 Wakorintho

2 Wakorintho 12

Maono Ya Paulo Na Mwiba Aliokuwa Nao

1 Yanipasa nijisifu, ingawa haifaidi kitu. Nitaenda kwenye maono na ufunuo kutoka kwa Bwana.

2 Namjua mtu mmoja katika Kristo ambaye miaka kumi na minne iliyopita alichukuliwa juu hadi mbingu ya tatu. Kama ni katika mwili au nje ya mwili, sijui, Mungu ajua.

3 Nami najua ya kwamba mtu huyu, kwamba ni katika mwili au nje ya mwili mimi sijui, lakini Mungu ajua,

4 alinyakuliwa hadi Paradiso.Huko alisikia mambo yasiyoelezeka, mambo ambayo binadamu hana ruhusa ya kuyasimulia.

5 Nitajisifu kwa ajili ya mtu kama huyo, lakini sitajisifu kuhusu mimi mwenyewe ila mimi nitajisifia udhaifu wangu.

6 Hata kama ningependa kujisifu, sitakuwa mjinga, kwa maana nitakuwa nasema kweli. Lakini najizuia, ili mtu yeyote asije akaniona mimi kuwa bora zaidi kuliko ninavyoonekana katika yale ninayotenda na kusema.

7 Ili kunizuia nisijivune kwa sababu ya ufunuo huu mkuu, nilipewa mwiba katika mwili wangu, mjumbe wa Shetani, ili anitese.

8 Kwa habari ya jambo hili nilimsihi Bwana mara tatu aniondolee mwiba huu.

9 Lakini aliniambia, “Neema yangu inakutosha, kwa kuwa uweza wangu hukamilika katika udhaifu.” Kwa hiyo nitajisifu kwa furaha zaidi kuhusu udhaifu wangu, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu.

10 Hii ndiyo sababu, kwa ajili ya Kristo, nafurahia udhaifu, katika kutukanwa, katika taabu, katika mateso na katika shida, kwa maana ninapokuwa dhaifu, ndipo nina nguvu.

Wasiwasi Wa Paulo Kwa Wakorintho

11 Nimekuwa mjinga, lakini ninyi mmenilazimisha niwe hivyo. Kwa kuwa ilinipasa kusifiwa na ninyi, kwa sababu mimi si dhalili kuliko wale “mitume walio bora,” ingawa mimi si kitu.

12 Mambo yanayomtambulisha mtume wa kweli, yaani, ishara, miujiza na maajabu, yalifanywa miongoni mwenu kwa saburi nyingi.

13 Je, ninyi ni kitu gani mlichopungukiwa kuliko makanisa mengine, ila tu kwamba mimi sikuwa mzigo kwenu? Nisameheni kwa kosa hili!

14 Sasa niko tayari kuja kwenu kwa mara hii ya tatu, nami sitawalemea, kwa sababu sitahitaji chochote chenu, ila ninawahitaji ninyi, kwa kuwa hata hivyo watoto hawaweki akiba kwa ajili ya wazazi wao, bali wazazi huweka akiba kwa ajili ya watoto wao.

15 Hivyo nitafurahi kutumia kila kitu nilicho nacho kwa ajili yenu, hata mwili wangu pia. Hata ingawa inaonekana ninavyozidi kuwapenda, ndivyo upendo wenu kwangu unavyopungua.

16 Iwe iwavyo, kwa vyovyote vile mimi sikuwalemea. Lakini kwa mimi kuwa mwerevu naliwapata.

17 Je, nilijipatia faida kwa kumtumia mtu yeyote niliyemtuma kwenu?

18 Nilimshawishi Tito aje kwenu, nami nilimtuma pamoja na ndugu yetu. Je, Tito aliwatumia ninyi ili kujipatia faida? Je, hatuenendi kwa roho moja, na hatuchukui hatua zile zile?

19 Je, mmekuwa mkifikiri kwamba sisi tunajaribu kujitetea mbele yenu? Sisi tumekuwa tukinena mbele za Mungu kama wale walio katika Kristo. Na chochote tufanyacho, ndugu wapendwa, ni kwa ajili ya kuwatia nguvu.

20 Kwa kuwa nina hofu ya kwamba nitakapokuja naweza kuwakuta nisivyotaka, nanyi mkanikuta msivyotaka. Nina hofu kwamba panaweza kuwa na ugomvi, wivu, ghadhabu, fitina, masingizio, masengenyo, majivuno na machafuko.

21 Nina hofu kwamba nitakapokuja tena kwenu, Mungu wangu atanidhili mbele yenu, nami nitasikitishwa na wengi waliotenda dhambi mbeleni, na wala hawajatubu kwa uchafu wao, uasherati, na ufisadi walioushiriki.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/2CO/12-24b1b54784eba08b21cb028284b1cb08.mp3?version_id=1627—

Categories
2 Wakorintho

2 Wakorintho 13

Maonyo Ya Mwisho

1 Hii ndiyo mara ya tatu mimi kuja kwenu. “Shtaka lolote lazima lithibitishwe na mashahidi wawili au watatu.”

2 Nimekwisha kuwaonya nilipokuwa pamoja nanyi mara ya pili. Sasa narudia wakati sipo, kwamba nikija tena sitawahurumia wale waliokuwa wametenda dhambi hapo awali na wengine wote,

3 kwa kuwa mnadai uthibitisho kwamba Kristo anazungumza kwa kunitumia mimi. Yeye si dhaifu katika kushughulika nanyi, bali ana nguvu kati yenu.

4 Kwa kuwa alisulubiwa katika udhaifu, lakini anaishi kwa nguvu za Mungu. Vivyo hivyo, sisi tu dhaifu kupitia kwake, lakini katika kuwashughulikia ninyi tutaishi pamoja naye kwa nguvu za Mungu.

5 Jichunguzeni wenyewe mwone kama mnaishi katika imani. Jipimeni wenyewe. Je, hamtambui ya kuwa Yesu Kristo yumo ndani yenu? Kama sivyo, basi, mmeshindwa kufikia kipimo hicho!

6 Natumaini mtaona kuwa sisi hatukushindwa.

7 Lakini tunamwomba Mungu msije mkatenda kosa lolote, si ili sisi tuonekane kuwa tumeshinda hilo jaribio, bali ili ninyi mtende lililo haki, hata kama tutaonekana kuwa tumeshindwa.

8 Kwa maana hatuwezi kufanya lolote kinyume na kweli, bali kuithibitisha kweli tu.

9 Tunafurahi wakati wowote sisi tunapokuwa dhaifu, lakini ninyi mkawa na nguvu. Nayo maombi yetu ni kwamba mpate kuwa wakamilifu.

10 Hii ndiyo sababu nawaandikia mambo haya wakati sipo, ili nikija nisiwe mkali katika kutumia mamlaka yangu, mamlaka Bwana aliyonipa ya kuwajenga ninyi wala si ya kuwabomoa.

Salamu Za Mwisho

11 Hatimaye, ndugu zangu, kwaherini. Kuweni wakamilifu, mkafarijike, kuweni wa nia moja, kaeni kwa amani. Naye Mungu wa upendo na amani atakuwa pamoja nanyi.

12 Salimianeni ninyi kwa ninyi kwa busu takatifu.

13 Watakatifu wote wanawasalimu.

14 Neema ya Bwana Yesu Kristo, na upendo wa Mungu, na ushirika wa Roho Mtakatifu ukae nanyi nyote. Amen.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/2CO/13-22f9965197caab0b1b9f7bf9f1d3b32e.mp3?version_id=1627—

Categories
Wagalatia

Wagalatia Utangulizi

Utangulizi

Paulo aliandika waraka huu katika safari yake ya kwanza ya kueneza Injili. Baada yake kuondoka Galatia, waumini Wayahudi walifika huko, nao wakaanza kusisitiza kwamba lazima watu wa Mataifa walioamini kwanza watimize Sheria ya Mose ili wapate kuokoka. Paulo aliandika kupinga mafundisho hayo, akionyesha jinsi Abrahamu, ambaye aliishi miaka 400 kabla ya Sheria ya Mose kutolewa, alivyookolewa kwa imani. Alionyesha kwamba kama vile Sheria haingeweza kumwokoa mtu, basi hakuna mtu angeweza kuwa mkamilifu kwa kujitahidi kwa uwezo wake mwenyewe kuitimiza Sheria.

Mwandishi

Mtume Paulo.

Kusudi

Kukataa mafundisho ya kuwa muumini wa Mataifa ni lazima atii sheria za Kiyahudi ndio aokolewe.

Wazo Kuu

Paulo anatetea kwa bidii kweli ya Injili ambayo kiini chake ni kwamba, “Mtu anaokolewa kwa neema ya Mungu kwa kumwamini Kristo.”

Mambo Muhimu

Paulo anasisitiza uhalali wa Injili, ubora wa Injili, na uhuru wa Injili.

Mahali

Antiokia.

Tarehe

Kama 49 B.K.

Wahusika Wakuu

Paulo, Tito, Barnaba, Petro, na walimu wa uongo.

Mgawanyo

Paulo atetea Injili na mamlaka yake kama mtume (

1:1–2:21

)

Kuwekwa huru kutokana na Sheria (

3:1-24

)

Ukuu wa Injili juu ya Sheria (

3:25–4:31

)

Uhuru wa Mkristo (

5:1-26

)

Mawaidha kuhusu mwenendo wa Mkristo (

6:1-18

).

Categories
Wagalatia

Wagalatia 1

Salamu

1 Paulo mtume: si mtume wa wanadamu wala aliyetumwa na mwanadamu, bali na Yesu Kristo na Mungu Baba aliyemfufua Yesu kutoka kwa wafu;

2 na ndugu wote walio pamoja nami:

Kwa makanisa ya Galatia:

3 Neema iwe nanyi na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana wetu Yesu Kristo,

4 aliyejitoa kwa ajili ya dhambi zetu ili apate kutuokoa katika ulimwengu huu wa sasa ulio mbaya, sawasawa na mapenzi yake yeye aliye Mungu na Baba yetu.

5 Utukufu una yeye milele na milele. Amen.

Hakuna Injili Nyingine

6 Nashangaa kwamba mnamwacha upesi hivyo yeye aliyewaita kwa neema ya Kristo na kuifuata Injili nyingine,

7 ambayo kwa kweli si Injili kamwe, ila kwa dhahiri kuna watu wanaowachanganya na wanaotaka kuipotosha Injili ya Kristo.

8 Lakini hata ikiwa sisi au malaika atokaye mbinguni akihubiri Injili nyingine tofauti na ile tuliyowahubiria sisi, basi mtu huyo alaaniwe milele!

9 Kama vile tulivyokwisha kusema kabla, sasa nasema tena, ikiwa mtu yeyote atawahubiria Injili kinyume na ile mliyoipokea na alaaniwe milele!

10 Je, sasa mimi ninatafuta kukubaliwa na wanadamu au kukubaliwa na Mungu? Au nataka kuwapendeza wanadamu? Kama ningekuwa bado najaribu kuwapendeza wanadamu, nisingekuwa mtumishi wa Kristo.

Paulo Ameitwa Na Mungu

11 Ndugu zangu, nataka mjue kwamba Injili niliyowahubiria haikutokana na wanadamu.

12 Kwa maana mimi sikuipokea hiyo Injili kutoka kwa mwanadamu, wala sikufundishwa na mtu, bali niliipata kwa ufunuo kutoka kwa Yesu Kristo.

13 Ninyi mmekwisha kusikia juu ya maisha yangu ya zamani nilipokuwa katika dini ya Kiyahudi, jinsi nilivyolitesa kanisa la Mungu kwa nguvu na kujaribu kuliangamiza.

14 Nami niliendelea sana katika dini ya Kiyahudi kuliko Wayahudi wengi wa rika yangu maana nilijitahidi sana katika desturi za baba zangu.

15 Lakini ilipompendeza Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu na kuniita kwa neema yake,

16 alimdhihirisha Mwanawe kwangu, ili nipate kumhubiri miongoni mwa watu wa Mataifa. Mimi sikushauriana na mwanadamu yeyote,

17 wala sikupanda kwenda Yerusalemu kuwaona hao waliokuwa mitume kabla yangu, bali nilikwenda mara moja Arabuni na kisha nikarudi Dameski.

18 Kisha baada ya miaka mitatu nilipanda kwenda Yerusalemu kuonana na Kefana nilikaa naye siku kumi na tano.

19 Lakini sikumwona mtume mwingine yeyote isipokuwa Yakobo, ndugu yake Bwana.

20 Nawahakikishia mbele za Mungu kuwa ninayowaandikia si uongo.

21 Baadaye nilikwenda sehemu za Syriana Kilikia.

22 Lakini mimi binafsi sikujulikana kwa makanisa ya huko Uyahudi yaliyo katika Kristo.

23 Wao walisikia habari tu kwamba, “Mtu yule ambaye hapo kwanza alikuwa akitutesa sasa anahubiri imani ile ile aliyokuwa akijaribu kuiangamiza.”

24 Nao wakamtukuza Mungu kwa sababu yangu.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/GAL/1-649c2f7f95ab2e700f543da9f9e1b989.mp3?version_id=1627—