Categories
Yeremia

Yeremia 9

1 Laiti kichwa changu kingekuwa chemchemi ya maji

na macho yangu yangekuwa kisima cha machozi!

Ningelia usiku na mchana

kwa kuuawa kwa watu wangu.

2 Laiti ningekuwa na nyumba

ya kukaa wasafiri jangwani,

ningewaacha watu wangu

na kwenda mbali nao,

kwa kuwa wote ni wazinzi,

kundi la watu wadanganyifu.

3 “Huweka tayari ndimi zao kama upinde,

ili kurusha uongo;

wamekuwa na nguvu katika nchi

lakini si katika ukweli.

Wanatoka dhambi moja hadi nyingine,

hawanitambui mimi,”

asemaBwana.

4 “Jihadhari na rafiki zako;

usiwaamini ndugu zako.

Kwa kuwa kila ndugu ni mdanganyifu,

na kila rafiki ni msingiziaji.

5 Rafiki humdanganya rafiki,

hakuna yeyote asemaye kweli.

Wamefundisha ndimi zao kudanganya,

wanajichosha wenyewe katika kutenda dhambi.

6 Unakaa katikati ya udanganyifu;

katika udanganyifu wao wanakataa kunitambua mimi,”

asemaBwana.

7 Kwa hiyo hili ndilo asemaloBwanaMwenye Nguvu Zote:

“Tazama, nitawasafisha na kuwajaribu,

kwani ni nini kingine niwezacho kufanya

kwa sababu ya dhambi ya watu wangu?

8 Ndimi zao ni mshale wenye sumu,

hunena kwa udanganyifu.

Kwa kinywa chake kila mmoja huzungumza maneno mazuri na jirani yake,

lakini moyoni mwake humtegea mtego.

9 Je, nisiwaadhibu kwa ajili ya jambo hili?”

asemaBwana.

“Je, nisijilipizie kisasi

kwa taifa kama hili?”

10 Nitalia na kuomboleza kwa ajili ya milima

na kuomboleza kuhusu malisho ya jangwani.

Yamekuwa ukiwa, wala hakuna apitaye humo,

milio ya ngʼombe haisikiki.

Ndege wa angani wametoroka

na wanyama wamekimbia.

11 “Nitaifanya Yerusalemu lundo la magofu,

makao ya mbweha;

nami nitaifanya miji ya Yuda kuwa ukiwa

ili asiwepo atakayeishi humo.”

12 Ni mtu yupi aliye na hekima ya kutosha ayaelewe haya? Ni nani aliyefundishwa naBwanaawezaye kuyaeleza haya? Kwa nini nchi imeharibiwa na kufanywa ukiwa kama jangwa ambapo hakuna awezaye kupita?

13 Bwanaakasema, “Ni kwa sababu wameiacha sheria yangu, niliyoiweka mbele yao: hawajaniheshimu mimi wala kufuata sheria yangu.

14 Badala yake wamefuata ukaidi wa mioyo yao, wamefuata Mabaali, kama vile baba zao walivyowafundisha.”

15 Kwa hiyo, hivi ndivyo asemavyoBwanaMwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli: “Tazama, nitawafanya watu hawa wale chakula kichungu na kunywa maji yenye sumu.

16 Nitawatawanya katika mataifa ambayo wao wala baba zao hawakuwajua, nikiwafuata kwa upanga mpaka niwe nimewaangamiza kabisa.”

17 Hivi ndivyo asemavyoBwanaMwenye Nguvu Zote:

“Fikiri sasa! Waite wanawake waombolezao waje,

waite wale walio na ustadi kuliko wote.

18 Nao waje upesi

na kutuombolezea,

mpaka macho yetu yafurike machozi

na vijito vya maji vitoke kwenye kope zetu.

19 Sauti ya kuomboleza imesikika kutoka Sayuni:

‘Tazama jinsi tulivyoangamizwa!

Tazama jinsi aibu yetu ilivyo kubwa!

Ni lazima tuihame nchi yetu

kwa sababu nyumba zetu zimekuwa magofu.’ ”

20 Basi, enyi wanawake, sikieni neno laBwana;

fungueni masikio yenu msikie maneno ya kinywa chake.

Wafundisheni binti zenu kuomboleza;

fundishaneni kila mmoja na mwenzake maombolezo.

21 Mauti imeingia ndani kupitia madirishani,

imeingia kwenye majumba yetu ya fahari;

imewakatilia mbali watoto katika barabara

na vijana waume kutoka viwanja vya miji.

22 Sema, “Hili ndilo asemaloBwana:

“ ‘Maiti za wanaume zitalala

kama mavi katika mashamba,

kama malundo ya nafaka nyuma ya mvunaji,

wala hakuna anayekusanya.’ ”

23 Hili ndilo asemaloBwana:

“Mwenye hekima asijisifu katika hekima yake,

au mwenye nguvu ajisifu katika nguvu zake,

wala tajiri ajisifu katika utajiri wake,

24 lakini yeye ajisifuye, na ajisifu kwa sababu hili:

kwamba ananifahamu na kunijua mimi,

kwamba mimi ndimiBwana, nitendaye wema,

hukumu na haki duniani,

kwa kuwa napendezwa na haya,”

asemaBwana.

25 “Siku zinakuja, nitakapowaadhibu wale wote ambao wametahiriwa kimwili tu, asemaBwana,

26 yaani Misri, Yuda, Edomu, Amoni, Moabu na wote wanaoishi jangwani sehemu za mbali. Kwa maana mataifa haya yote hayakutahiriwa mioyo yao, nayo nyumba yote ya Israeli haikutahiriwa.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JER/9-2849268e2ce5e5921009817933f8b1bf.mp3?version_id=1627—

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *