Categories
Yeremia

Yeremia 31

Mahamisho Kurudi Kwa Shangwe

1 “Wakati huo, nitakuwa Mungu wa koo zote za Israeli nao watakuwa watu wangu,” asemaBwana.

2 Hili ndilo asemaloBwana:

“Watu watakaopona upanga

watapata upendeleo jangwani;

nitakuja niwape Israeli pumziko.”

3 Bwanaalitutokea wakati uliopita, akisema:

“Nimekupenda kwa upendo wa milele,

nimekuvuta kwa wema.

4 Nitakujenga tena nawe utajengeka upya,

ewe Bikira Israeli.

Utachukua tena matari yako

na kwenda kucheza na wenye furaha.

5 Utapanda tena shamba la mizabibu

juu ya vilima vya Samaria,

wakulima watapanda

na kufurahia matunda yake.

6 Itakuja siku wakati walinzi watakapowapigia kelele

juu ya vilima vya Efraimu wakisema,

‘Njooni, twendeni juu Sayuni,

kwakeBwanaMungu wetu.’ ”

7 Hili ndilo asemaloBwana:

“Mwimbieni Yakobo kwa furaha,

mpigieni kelele aliye mkuu wa mataifa.

Zifanyeni sifa zenu zisikike, nanyi mseme,

‘EeBwana, okoa watu wako,

mabaki ya Israeli.’

8 Tazama, nitawaleta kutoka nchi ya kaskazini

na kuwakusanya kutoka miisho ya dunia.

Miongoni mwao watakuwepo vipofu na viwete,

mama wajawazito na wenye utungu wa kuzaa.

Umati mkubwa wa watu utarudi.

9 Watakuja wakilia;

wataomba wakati ninawarudisha.

Nitawaongoza kando ya vijito vya maji

katika mapito yaliyo tambarare ambapo hawatajikwaa,

kwa sababu mimi ndimi baba wa Israeli,

naye Efraimu ni mzaliwa wangu wa kwanza.

10 “Sikieni neno laBwana, enyi mataifa,

litangazeni katika nchi za pwani ya mbali:

‘Yeye aliyewatawanya Israeli atawakusanya

na atalichunga kundi lake la kondoo kama mchungaji.’

11 Kwa kuwaBwanaatamlipia fidia Yakobo

na kuwakomboa mkononi mwa walio na nguvu kuliko wao.

12 Watakuja na kupiga kelele kwa furaha katika miinuko ya Sayuni;

watashangilia ukarimu waBwana:

nafaka, divai mpya na mafuta,

wana-kondoo wachanga

na ndama wa makundi ya ngʼombe nitakaowapa.

Watakuwa kama bustani iliyonyeshewa vizuri,

wala hawatahuzunika tena.

13 Kisha wanawali watacheza na kufurahi,

vijana waume na wazee pia.

Nitageuza maombolezo yao kuwa furaha,

nitawapa faraja na furaha badala ya huzuni.

14 Nitawashibisha makuhani kwa wingi,

nao watu wangu watajazwa kwa ukarimu wangu,”

asemaBwana.

15 Hili ndilo asemaloBwana:

“Sauti imesikika huko Rama,

maombolezo na kilio kikubwa,

Raheli akiwalilia watoto wake

na anakataa kufarijiwa,

kwa sababu watoto wake hawako tena.”

16 Hili ndilo asemaloBwana:

“Izuie sauti yako kulia,

na macho yako yasitoe machozi,

kwa kuwa kazi yako itapata thawabu,”

asemaBwana.

“Watarudi kutoka nchi ya adui.

17 Kwa hiyo kuna tumaini kwa siku zijazo,”

asemaBwana.

“Watoto wako watarudi nchi yao yenyewe.

18 “Hakika nimeyasikia maombolezo ya Efraimu:

‘Ulinirudi kama ndama mkaidi,

nami nimekubali kutii.

Unirudishe, nami nitarudi,

kwa sababu wewe ndiweBwana, Mungu wangu.

19 Baada ya kupotea, nilitubu;

baada ya kuelewa, nilijipiga kifua.

Niliaibika na kuona haya

kwa sababu niliibeba aibu ya ujana wangu.’

20 Je, Efraimu si mwanangu mpendwa,

mtoto ninayependezwa naye?

Ingawa mara kwa mara ninanena dhidi yake,

bado ninamkumbuka.

Kwa hiyo moyo wangu unamwonea shauku,

nina huruma kubwa kwa ajili yake,”

asemaBwana.

21 “Weka alama za barabara,

weka vibao vya kuelekeza.

Zingatia vyema njia kuu,

barabara ile unayoipita.

Rudi, ee Bikira Israeli,

rudi kwenye miji yako.

22 Utatangatanga hata lini,

ee binti usiye mwaminifu?

Bwanaameumba kitu kipya duniani:

mwanamke atamlinda mwanaume.”

23 Hili ndiloBwanaMwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo, “Nitakapowarudisha toka nchi ya kutekwa kwenu, watu walio katika nchi ya Yuda na miji yake kwa mara nyingine tena watatumia maneno haya: ‘Bwanaakubariki, ee makao ya haki, ee mlima mtakatifu.’

24 Watu wataishi pamoja katika Yuda na miji yake yote, wakulima na wote wanaohamahama na mifugo yao.

25 Nitawaburudisha waliochoka na kuwatuliza walio na huzuni.”

26 Kwa jambo hili niliamka na kuangalia pande zote. Usingizi wangu ulikuwa mtamu kwangu.

27 Bwanaasema, “Siku zinakuja, nitakapoongeza idadi ya watu, na kuzidisha hesabu ya mifugo katika nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda.

28 Kama vile nilivyowaangalia ili kungʼoa na kubomoa, kuharibu, kuangamiza na kuleta maafa juu yao, vivyo hivyo nitawaangalia ili kujenga na kupanda,” asemaBwana.

29 “Katika siku hizo, watu hawatasema tena,

“ ‘Baba wamekula zabibu chachu,

nayo meno ya watoto yakatiwa ganzi.’

30 Badala yake, kila mmoja atakufa kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe; yeyote alaye zabibu chachu, meno yake mwenyewe yatatiwa ganzi.

31 “Siku zinakuja,” asemaBwana,

“nitakapofanya agano jipya

na nyumba ya Israeli

na nyumba ya Yuda.

32 Halitafanana na agano

nililofanya na baba zao

wakati nilipowashika mkono

kuwaongoza watoke Misri,

kwa sababu walivunja agano langu,

ijapokuwa nilikuwa mume kwao,”

asemaBwana.

33 “Hili ndilo agano nitakalofanya na nyumba ya Israeli

baada ya siku zile,” asemaBwana.

“Nitaweka sheria yangu katika nia zao,

na kuiandika mioyoni mwao.

Nitakuwa Mungu wao,

nao watakuwa watu wangu.

34 Mtu hatamfundisha tena jirani yake,

wala mtu kumfundisha ndugu yake akisema, ‘MjueBwanaMungu,’

kwa sababu wote watanijua mimi,

tangu aliye mdogo kabisa kwao, hadi aliye mkuu sana,”

asemaBwana.

“Kwa sababu nitasamehe uovu wao,

wala sitazikumbuka dhambi zao tena.”

35 Hili ndilo asemaloBwana,

yeye aliyeweka jua

liwake mchana,

yeye anayeamuru mwezi na nyota

kungʼaa usiku,

yeye aichafuaye bahari

ili mawimbi yake yangurume;

BwanaMwenye Nguvu Zote ndilo jina lake:

36 “Ikiwa amri hizi zitaondoka machoni pangu,”

asemaBwana,

“ndipo wazao wa Israeli watakoma

kuwa taifa mbele yangu daima.”

37 Hili ndilo asemaloBwana:

“Ikiwa mbingu zilizo juu zitaweza kupimika

na misingi ya dunia chini

ikaweza kuchunguzwa,

ndipo nitakapowakataa wazao wote wa Israeli

kwa sababu ya yote waliyoyatenda,”

asemaBwana.

38 “Siku zinakuja,” asemaBwana, “wakati mji huu utajengwa upya kwa ajili yangu, kuanzia mnara wa Hananeli hadi Lango la Pembeni.

39 Kamba ya kupimia itaanzia hapo kuendelea hadi kwenye kilima cha Garebu, na kisha kugeuka kuelekea Goa.

40 Bonde lote watupwapo maiti na majivu pia na matuta yote kutoka Bonde la Kidroni upande wa mashariki hadi pembe ya Lango la Farasi, itakuwa takatifu kwaBwana. Kamwe mji huu hautangʼolewa tena wala kubomolewa.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/JER/31-9fa262e701d74299e658fe94c13bfda7.mp3?version_id=1627—

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *