Categories
Isaya

Isaya 51

Wokovu Wa Milele Kwa Sayuni

1 “Nisikilizeni, ninyi mnaofuatia haki

na mnaomtafutaBwana:

Tazameni mwamba ambako mlichongwa,

na mahali pa kuvunjia mawe ambako mlichimbwa;

2 mwangalieni Abrahamu, baba yenu,

na Sara, ambaye aliwazaa.

Wakati nilipomwita alikuwa mmoja tu,

nami nikambariki na kumfanya kuwa wengi.

3 HakikaBwanaataifariji Sayuni,

naye atayaangalia kwa huruma magofu yake yote;

atayafanya majangwa yake yawe kama Edeni,

nazo sehemu zake zisizolimika ziwe kama bustani yaBwana.

Shangwe na furaha zitakuwako ndani yake,

shukrani na sauti za kuimba.

4 “Nisikilizeni, watu wangu;

nisikieni, taifa langu:

Sheria itatoka kwangu;

haki yangu itakuwa nuru kwa mataifa.

5 Haki yangu inakaribia mbio,

wokovu wangu unakuja,

nao mkono wangu utaleta hukumu kwa mataifa.

Visiwa vitanitegemea

na kungojea mkono wangu kwa matumaini.

6 Inueni macho yenu mbinguni,

mkaitazame dunia chini;

mbingu zitatoweka kama moshi,

dunia itachakaa kama vazi,

na wakazi wake kufa kama mainzi.

Bali wokovu wangu utadumu milele,

haki yangu haitakoma kamwe.

7 “Nisikieni, ninyi mnaojua lililo sawa,

ninyi watu ambao mna sheria yangu mioyoni mwenu:

Msiogope mashutumu ya wanadamu

wala msitiwe hofu na matukano yao.

8 Kwa maana nondo atawala kama vazi,

nao funza atawatafuna kama sufu.

Lakini haki yangu itadumu milele,

wokovu wangu kwa vizazi vyote.”

9 Amka, Amka! Jivike nguvu,

ewe mkono waBwana,

Amka, kama siku zilizopita,

kama vile vizazi vya zamani.

Si ni wewe uliyemkata Rahabu vipande vipande,

uliyemchoma yule joka?

10 Si ni wewe uliyekausha bahari,

maji ya kilindi kikuu,

uliyefanya barabara katika vilindi vya bahari

ili waliokombolewa wapate kuvuka?

11 Wale waliolipiwa fidia naBwanawatarudi.

Wataingia Sayuni wakiimba;

furaha ya milele itakuwa taji juu ya vichwa vyao.

Furaha na shangwe zitawapata,

huzuni na kulia kwa uchungu kutatoweka.

12 “Mimi, naam mimi,

ndimi niwafarijie ninyi.

Ninyi ni nani hata kuwaogopa

wanadamu wanaokufa,

wanadamu ambao ni majani tu,

13 kwamba mnamsahauBwanaMuumba wenu,

aliyezitanda mbingu

na kuiweka misingi ya dunia,

kwamba mnaishi katika hofu siku zote

kwa sababu ya ghadhabu ya mdhalimu,

ambaye nia yake ni kuangamiza?

Iko wapi basi ghadhabu ya mdhalimu?

14 Wafungwa waliojikunyata kwa hofu

watawekwa huru karibuni;

hawatafia kwenye gereza lao,

wala hawatakosa chakula.

15 Kwa maana Mimi ndimiBwana, Mungu wako,

ambaye huisukasuka bahari ili mawimbi yake yangurume:

BwanaMwenye Nguvu Zote ndilo jina lake.

16 Nimeweka maneno yangu kinywani mwako

na kukufunika kwa uvuli wa mkono wangu:

Mimi niliyeweka mbingu mahali pake,

niliyeweka misingi ya dunia,

niwaambiaye Sayuni,

‘Ninyi ni watu wangu.’ ”

Kikombe Cha Ghadhabu Ya Bwana

17 Amka, amka!

Simama, ee Yerusalemu,

wewe uliyekunywa kutoka mkono waBwana

kikombe cha ghadhabu yake,

wewe uliyekunywa mpaka kufikia machujo yake,

kikombe kile cha kunywea

kiwafanyacho watu kuyumbayumba.

18 Kati ya wana wote aliowazaa

hakuwepo hata mmoja wa kumwongoza,

kati ya wana wote aliowalea

hakuwepo hata mmoja wa kumshika mkono.

19 Majanga haya mawili yamekuja juu yako:

ni nani awezaye kukufariji?

Maangamizi, uharibifu, njaa na upanga:

ni nani awezaye kukutuliza?

20 Wana wako wamezimia,

wamelala kwenye mwanzo wa kila barabara,

kama swala aliyenaswa kwenye wavu.

Wamejazwa na ghadhabu yaBwana

na makaripio ya Mungu wako.

21 Kwa hiyo sikiliza hili, wewe uliyeteswa,

uliyelewa, lakini si kwa mvinyo.

22 Hili ndilo asemaloBwanaMwenyezi wako,

Mungu wako, yeye ambaye huwatetea watu wake:

“Tazama, nimeondoa mkononi mwako

kikombe kilichokufanya uyumbayumbe;

kutoka kikombe hicho,

kikombe cha kunywa cha ghadhabu yangu,

kamwe hutakunywa tena.

23 Nitakiweka mikononi mwa watesi wako,

wale waliokuambia,

‘Anguka kifudifudi

ili tuweze kutembea juu yako.’

Ukaufanya mgongo wako kama ardhi,

kama njia yao ya kupita.”

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/51-f745b61a926dc7b2dcdcd68d4df3598b.mp3?version_id=1627—

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *