Categories
Isaya

Isaya 46

Miungu Ya Babeli

1 Beli anasujudu hadi nchi, Nebo anainama;

sanamu zao zabebwa na wanyama wa mizigo.

Vinyago hivi mnavyobeba kila mahali ni mzigo wa kulemea,

mzigo kwa waliochoka.

2 Vinyago pamoja na wale wanaovibeba wanainama chini;

hiyo miungu haiwezi kuwaokoa watu,

wote wanakwenda utumwani pamoja.

3 “Nisikilizeni mimi, ee nyumba ya Yakobo,

ninyi nyote mliobaki wa nyumba ya Israeli,

ninyi ambao nimewategemeza tangu mlipotungwa mimba,

nami nimewabeba tangu kuzaliwa kwenu.

4 Hata mpaka wakati wa uzee wenu na mvi, Mimi ndiye,

Mimi ndiye nitakayewasaidia ninyi.

Nimewahuluku, nami nitawabeba,

nitawasaidia ninyi na kuwaokoa.

5 “Mtanilinganisha na nani, au mtanihesabu kuwa sawa na nani?

Ni nani mtakayenifananisha naye ili tuweze kulinganishwa?

6 Wengine humwaga dhahabu kutoka kwenye mifuko yao,

na kupima fedha kwenye mizani;

huajiri mfua dhahabu kutengeneza mungu,

kisha huisujudia na kuiabudu.

7 Huiinua mabegani na kuichukua;

huiweka mahali pake, papo hapo ndipo isimamapo.

Wala haiwezi kusogea kutoka mahali pale.

Ingawa mtu huililia, haimjibu;

haiwezi kumwokoa kwenye taabu zake.

8 “Kumbukeni hili, litieni akilini,

liwekeni moyoni, enyi waasi.

9 Kumbukeni mambo yaliyopita, yale ya zamani za kale;

mimi ndimi Mungu, wala hakuna mwingine;

mimi ndimi Mungu,

wala hakuna mwingine aliye kama mimi.

10 Ni mimi nitangazaye mwisho tangu mwanzo,

naam, tangu zamani za kale,

mambo ambayo hayajatendeka.

Ninasema: Kusudi langu ndilo litakalosimama,

nami nitatenda mapenzi yangu yote.

11 Kutoka mashariki ninaita ndege awindaye;

kutoka nchi ya mbali,

mtu atakayetimiza kusudi langu.

Lile ambalo nimelisema, ndilo nitakalolitimiza;

lile nililolipanga, ndilo nitakalolitenda.

12 Nisikilizeni, ninyi wenye mioyo migumu,

ninyi mlio mbali na haki.

13 Ninaleta haki yangu karibu,

haiko mbali;

wala wokovu wangu hautachelewa.

Nitawapa Sayuni wokovu,

Israeli utukufu wangu.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/46-eac1d24dd960b072cef119ad4ac2543f.mp3?version_id=1627—

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *