Categories
Isaya

Isaya 22

Unabii Kuhusu Yerusalemu

1 Neno kuhusu Bonde la Maono:

Nini kinachokutaabisha sasa,

kwamba ninyi nyote mmepanda juu ya mapaa?

2 Ewe mji uliojaa ghasia,

ewe mji wa makelele na sherehe!

Watu wenu waliokufa hawakuuawa kwa upanga,

wala hawakufa vitani.

3 Viongozi wako wote wamekimbia pamoja,

wamekamatwa bila kutumia upinde.

Ninyi nyote mliokamatwa mlichukuliwa wafungwa pamoja,

mlikimbia wakati adui alipokuwa bado mbali.

4 Kwa hiyo nilisema, “Geukia mbali nami,

niache nilie kwa uchungu.

Usijaribu kunifariji

juu ya maangamizi ya watu wangu.”

5 Bwana,BwanaMwenye Nguvu Zote, anayo siku

ya ghasia, ya kukanyaga, na ya kuogofya

katika Bonde la Maono,

siku ya kuangusha kuta

na ya kupiga kelele mpaka milimani.

6 Elamu analichukua podo,

pamoja na waendesha magari ya vita na farasi.

Kiri anaifungua ngao.

7 Mabonde yako yaliyo mazuri sana yamejaa magari ya vita,

nao wapanda farasi wamewekwa kwenye malango ya mji;

8 ulinzi wa Yuda umeondolewa.

Nawe ulitazama siku ile

silaha katika Jumba la Kifalme la Mwituni,

9 mkaona kuwa Mji wa Daudi

una matundu mengi katika ulinzi wake,

mkaweka akiba ya maji

kwenye Bwawa la Chini.

10 Mlihesabu majengo katika Yerusalemu

nanyi mkabomoa nyumba ili kuimarisha ukuta.

11 Mlijenga bwawa la maji katikati ya kuta mbili

kwa ajili ya maji ya Bwawa la Zamani,

lakini hamkumtazama Yule aliyelitengeneza,

au kuwa na heshima kwa Yule aliyeubuni tangu zamani za kale.

12 Bwana,BwanaMwenye Nguvu Zote,

aliwaita siku ile

ili kulia na kuomboleza,

kungʼoa nywele zenu na kuvaa nguo ya gunia.

13 Lakini tazama, kuna furaha na sherehe,

kuchinja ngʼombe na kuchinja kondoo,

kula nyama na kunywa mvinyo!

Mnasema, “Tuleni na kunywa,

kwa kuwa kesho tutakufa!”

14 BwanaMwenye Nguvu Zote amelifunua hili nikiwa ninasikia: Bwana,BwanaMwenye Nguvu Zote, asema: “Mpaka siku ya kufa kwenu, dhambi hii haitafanyiwa upatanisho.”

15 Hili ndilo Bwana,BwanaMwenye Nguvu Zote, asemalo:

“Nenda ukamwambie huyu wakili Shebna,

ambaye ni msimamizi wa jumba la kifalme:

16 Unafanya nini hapa, na ni nani aliyekupa ruhusa

kujikatia kaburi lako mwenyewe,

ukichonga kaburi lako mahali palipo juu,

na kutoboa kwa patasi mahali pako pa kupumzikia katika mwamba?

17 “Jihadhari,Bwanayu karibu kukukamata thabiti,

na kukutupa mbali, ewe mtu mwenye nguvu.

18 Atakuvingirisha uwe kama mpira

na kukutupa katika nchi kubwa.

Huko ndiko utakakofia,

na huko ndiko magari yako ya vita ya fahari yatabakia,

wewe unayeifedhehesha nyumba ya bwana wako!

19 Nitakuondoa kutoka kazi yako,

nawe utaondoshwa kutoka nafasi yako.

20 “Katika siku ile, nitamwita mtumishi wangu, Eliakimu mwana wa Hilkia.

21 Nitamvika joho lako, nami nitamfunga mshipi wako kiunoni mwake, na kumkabidhi mamlaka yako. Yeye atakuwa baba kwa wale wanaoishi Yerusalemu na kwa nyumba ya Yuda.

22 Nitaweka mabegani mwake ufunguo wa nyumba ya Daudi. Kile afunguacho hakuna awezaye kufunga, na kile afungacho hakuna awezaye kufungua.

23 Nitamgongomea kama kigingi kilicho mahali palipo imara, naye atakuwa kiti cha enzi cha heshima kwa ajili ya nyumba ya baba yake.

24 Utukufu wote wa jamaa yake utakuwa juu yake: Watoto wa jamaa hiyo na machipukizi yake, vyombo vyake vyote vidogo, tangu bakuli hadi magudulia yote.”

25 BwanaMwenye Nguvu Zote asema, “Katika siku ile, kigingi kilichogongomewa mahali imara kitaachia njia. Kitakatwa, nacho kitaanguka na mzigo ulioningʼinia juu yake utaanguka chini.”Bwanaamesema.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/22-adb9150a718fe6572b0ba7194db44151.mp3?version_id=1627—

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *