Unabii Kuhusu Misri
1 Neno kuhusu Misri:
Tazama,Bwanaamepanda juu ya wingu liendalo kwa haraka
naye anakuja Misri.
Sanamu za Misri zinatetemeka mbele yake,
nayo mioyo ya Wamisri inayeyuka ndani yao.
2 “Nitamchochea Mmisri dhidi ya Mmisri,
ndugu atapigana dhidi ya ndugu,
jirani dhidi ya jirani,
mji dhidi ya mji,
ufalme dhidi ya ufalme.
3 Wamisri watakufa moyo,
na nitaibatilisha mipango yao.
Watatafuta ushauri kwa sanamu na kwa roho za waliokufa,
kwa waaguzi na kwa wale waongeao na mizimu.
4 Nitawatia Wamisri
mikononi mwa bwana mkatili
na mfalme mkali atatawala juu yao,”
asema Bwana,BwanaMwenye Nguvu Zote.
5 Maji ya mito yatakauka,
chini ya mto kutakauka kwa jua.
6 Mifereji itanuka;
vijito vya Misri vitapungua
na kukauka.
Mafunjo na nyasi vitanyauka,
7 pia mimea iliyoko kando ya Mto Naili,
pale mto unapomwaga maji baharini.
Kila shamba lililopandwa kando ya Mto Naili litakauka,
litapeperushwa na kutoweka kabisa.
8 Wavuvi watalia na kuomboleza,
wale wote watupao ndoano katika Mto Naili,
watadhoofika kwa majonzi.
9 Wale watu wafanyao kazi ya kitani kilichochambuliwa watakata tamaa,
wafumaji wa kitani safi watavunjika moyo.
10 Wafanyao kazi ya kufuma nguo watahuzunishwa,
nao vibarua wataugua moyoni.
11 Maafisa wa Soani ni wapumbavu kabisa,
washauri wa Farao wenye busara wanatoa ushauri wa kijinga.
Unawezaje kumwambia Farao,
“Mimi ni mmojawapo wa watu wenye hekima,
mwanafunzi wa wafalme wa zamani”?
12 Wako wapi sasa watu wako wenye hekima?
Wao wakuonyeshe na kukufahamisha
ni niniBwanaMwenye Nguvu Zote
amepanga dhidi ya Misri.
13 Maafisa wa Soani wamekuwa wapumbavu,
viongozi wa Memfisiwamedanganyika,
walio mawe ya pembe ya taifa lake
wameipotosha Misri.
14 Bwanaamewamwagia
roho ya kizunguzungu;
wanaifanya Misri iyumbayumbe
katika yale yote inayoyafanya,
kama vile mlevi ayumbayumbavyo
katika kutapika kwake.
15 Misri haiwezi kufanya kitu chochote,
cha kichwa wala cha mkia,
cha tawi la mtende wala cha tete.
16 Katika siku ile Wamisri watakuwa kama wanawake. Watatetemeka kwa hofu mbele ya mkono waBwanaMwenye Nguvu Zote anaoinua dhidi yao.
17 Nayo nchi ya Yuda itawatia hofu Wamisri, kila mmoja atakayetajiwa Yuda ataingiwa na hofu, kwa sababu ya kile ambachoBwanaMwenye Nguvu Zote anapanga dhidi yao.
18 Katika siku hiyo miji mitano ya Misri, itazungumza lugha ya Kanaani, na kuapa kumtiiBwanaMwenye Nguvu Zote. Mji mmojawapo utaitwa Mji wa Uharibifu.
19 Katika siku hiyo patakuwepo madhabahu yaBwanakatikati ya Misri na mnara wa kumbukumbu kwaBwanakwenye mpaka wa Misri.
20 Itakuwa alama na ushahidi kwa ajili yaBwanaMwenye Nguvu Zote katika nchi ya Misri. WatakapomliliaBwanakwa sababu ya watesi wao, Mungu atawapelekea mwokozi na mtetezi, naye atawaokoa.
21 HivyoBwanaatajijulisha mwenyewe kwa Wamisri, nao katika siku hiyo watamkubaliBwana. Wataabudu kwa kumtolea dhabihu na sadaka za nafaka, watamwekeaBwananadhiri na kuzitimiza.
22 Bwanaataipiga Misri kwa tauni; atawapiga na kuwaponya. WatamgeukiaBwana, naye atayasikia maombi yao na kuwaponya.
23 Katika siku hiyo kutakuwepo na njia kuu kutoka Misri hadi Ashuru. Waashuru watakwenda Misri, na Wamisri watakwenda Ashuru. Wamisri na Waashuru wataabudu pamoja.
24 Katika siku hiyo Israeli itakuwa ya tatu, pamoja na Misri na Ashuru, nao watakuwa baraka kwa dunia.
25 BwanaMwenye Nguvu Zote atawabariki, akisema, “Baraka iwe kwa Misri watu wangu, kwa Ashuru kazi ya mikono yangu, na kwa Israeli urithi wangu.”
—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/19-7e69346dd835d2fc7178455831747681.mp3?version_id=1627—