Categories
Isaya

Isaya 17

Neno Dhidi Ya Dameski

1 Neno kuhusu Dameski:

“Tazama, Dameski haitakuwa tena mji

bali itakuwa lundo la magofu.

2 Miji ya Aroeri itaachwa

na itaachiwa mifugo ambayo italala huko,

bila yeyote wa kuyaogopesha.

3 Mji wenye ngome utatoweka kutoka Efraimu,

nao uweza wa ufalme kutoka Dameski;

mabaki ya Aramu yatakuwa

kama utukufu wa Waisraeli,”

asemaBwanaMwenye Nguvu Zote.

4 “Katika siku ile utukufu wa Yakobo utafifia,

unono wa mwili wake utadhoofika.

5 Itakuwa kama mvunaji akusanyavyo nafaka

na kuvuna nafaka kwa mikono yake,

kama wakati mtu aokotapo masazo ya masuke

katika Bonde la Warefai.

6 Hata hivyo baadhi ya masazo yatabaki,

kama vile mti wa mzeituni unavyopigwa,

kukiachwa zeituni mbili au tatu juu ya matawi kileleni,

nne au tano katika matawi yazaayo sana,”

asemaBwana, Mungu wa Israeli.

7 Katika siku ile watu watamwangalia Muumba wao,

na kuelekeza macho yao kwa yule Aliye Mtakatifu wa Israeli.

8 Hawataziangalia tena madhabahu,

kazi za mikono yao,

nao hawataheshimu nguzo za Ashera,

na madhabahu za kufukizia uvumba zilizofanywa kwa mikono yao.

9 Katika siku ile miji yao iliyo imara, ambayo waliihama kwa sababu ya Waisraeli, itakuwa kama mahali palipoachwa pa vichaka na magugu. Nayo yote itakuwa ukiwa.

10 Mmemsahau Mungu Mwokozi wenu,

hamkumkumbuka Mwamba aliye ngome yenu.

Kwa hiyo, hata ingawa mlipandikiza mimea iliyo mizuri sana

na kuotesha mizabibu ya kigeni,

11 hata kama siku ile unapoipandikiza, unaifanya iote

na asubuhi ile ile unayoipanda, unaifanya ichipue,

hata hivyo mavuno yatakuwa kama si kitu

katika siku ile ya ugonjwa na maumivu yasiyoponyeka.

12 Lo! Ghadhabu ya mataifa mengi,

wanaghadhibika kama bahari iliyochafuka!

Lo! Makelele ya mataifa

wanavuma kama ngurumo za maji mengi!

13 Ingawa mataifa yanavuma kama ngurumo za maji yanayofanya mawimbi,

wakati anapoyakemea yanakimbia mbali,

yanafukuzwa mbele ya upepo kama makapi juu ya milima,

kama jani livingirishwapo na dhoruba.

14 Wakati wa jioni, hofu ya ghafula!

Kabla ya asubuhi, wametoweka!

Hili ndilo fungu la wale wanaotupora,

fungu la wale wanaotunyangʼanya mali zetu.

—https://api-cdn.youversionapi.com/audio-bible-youversionapi/337/32k/ISA/17-04b51c536a0dc3a1618bb7b3188095e8.mp3?version_id=1627—

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *